MKUU WA WILAYA TUNDURU AZINDUA UPIGAJI CHAPA NG'OMBE
Katika kutekeleza kwa vitendo sheria ya utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo namba 12 ya mwaka 2010 sambamba na kanuni zake za mwaka 2011 halmashauri ya wilaya ya Tunduru imefanya uzinduzi wa upigaji chapa ng’ombe mapema wiki hii katika Kijiji cha Muhuwesi ambapo mgeni rasmi alikuwa mkuu wa wilaya ya Tunduru Mh.Juma Zuberi Homera.
Akisoma taarifa ya uzinduzi wa zoezi hilo la upigaji chapa ng’ombe,Afisa Mifugo na Uvuvi wilaya Dk Frank Mkoma alisema wilaya ya Tunduru ina jumla ya ng’ombe 62,685, mbuzi 5,974, kondoo 3,388 na nguruwe 2,650. Kati ya vijiji 157 vya wilaya ya tunduru ni vijiji 41 vilivyokwisha kufanyiwa matumizi bora ya ardhi na jumla ya hekta 11,480 zimetengwa kwa ajili ya malisho, eneo hili lina uwezo wa kulisha mifugo 11,480.
Dk Mkoma alisema Halmashauri kwa awamu ya kwanza wanatarajia kupiga chapa ng’ombe wapatao 62,685 na watapigwa chapa kwenye mguu wa nyuma upande wa kulia.
“Katika zoezi hili la upigaji chapa ng’ombe, wafugaji wote wa ngombe waliopo kwenye wilaya kuanzia mwenye ng’ombe mmoja hadi makundi makubwa watahusika, na maeneo yenye mifugo mingi ni yale yaliyopo pembezoni hasa katika kata ya Ngapa, Mkowela, Twendembele Na Misechela.”alisema Dk Mkoma.
Aliendelea kusema kuwa kupiga chapa ng’ombe kuna faida hasa katika suala zima la ufuatiliaji, usajili na utambuzi wa mifugo kwani huzuia wizi wa mifugo na uhamishaji wa mifugo usiofuata taratibu za kisheria hasa kwa wafugaji wenye makundi makubwa ambao uhama toka sehemu moja kwenda nyingine kutafuta malisho bila kuwa na vibali vya kusafirishia mifugo.
Kwa upande wa wafugaji walioshiriki katika zoezi la upigaji chapa ng’ombe walishukuru serikali kwa kutambua umuhimu wa kufanya utambuzi wa ngombe na pia wanaiomba serikali kuwatengea maeneo yenye malisho ya kutosha na kuwajengea miundombinu ili waweze kufuga kisasa.
“sisi tuko tayari kuhamia katika maeneo ambayo serikali imepanga kutupeleka ili kuondoa migogoro kati ya wakulima na wafugaji kwa sababu sasa hivi tunalisha katika mashamba ya wakulima na wakati mwingine tunaingia katika hifadhi hivyo kugomba na maliasili na wakulima kutokana na mazao yao kuliwa na mifugo yetu”alisema Mfugaji Songambele Lereshi.
Naye mfugaji Nyengela Msafiri alisema kuwa wananenda kulisha katika mashamba ya wakulima na katika hifadhi za taifa na misitu ya jamii kutokana na maeneo waliyotengewa hayatoshelezi kwa malisho ya mifugo yao kutokana na nyasi kukauka hasa kipindi cha kiangazi.
Naye mkuu wa wilaya ya Tunduru Mh Juma Zuberi Homera ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo wa zoezi la kupiga chapa ng’ombe ni utekelezaji wa ilani ya chama cha mapinduzi ya mwaka 2015 ya kupunguza migogoro kati ya wakulima na wafugaji, na pia kufanya ufugaji wa kisasa.
Aidha homera aliendelea kusema kuwa serikali imekuwa ikishirikiana na shirika la dini la AMCC ambao wanatekeleza mradi katika wilaya ya tunduru na wanaprogramu ya kopa ng’ombe lipa ng’ombe ambao wanatoa mifugo ya mbuzi na ng’ombe kwa wananchi.
“kwa mwaka 2016 AMCC kupitia mradi wa CHIP walitoa ngombe 45 na mbuzi 60 na kwa mwaka huu 2017 wanatarajia kutoa ng’ombe 100 na mbuzi 120”
Aliendelea kusema kuwa maeneo yaliyotengwa na serikali kwa ajili ya kupeleka mifugo hasa kwa wafugaji wenye makundi makubwa ya ng’ombe ni Mkowela, Ngapa na Liwangula na wafugaji ambao mifugo yao itapigwa chapa ndio ambao wataanza kuelekezwa kuelekea huko.
Mkuu wa wilaya aliomba ushirikiano toka kwa wafugaji ili wananchi waweze kuishi kwa Amani na pia aliwataka wafugaji kufuata sheria, kanuni na taratibu za vijiji husika wanapoishi ili kuondoa migogoro kati ya mkulima na mfugaji wakati serikali ikiendelea na mipango ya kuwatengea maeneo na kuboresha miundombinu.
Alitoa rai kwa wafugaji ambao hawajajitokeza katika zoezi hilo wafanye hivyo kwani wilaya ya Tunduru haipo tayari kuendelea kuishi nao na kama watagoma mpaka zoezi litakapokamilika tarehe 26/10/2017 basi waondoke katika maeneo ya Tunduru.
Mh. Homera alimazia kwa kutoa rai kwa wafugaji wote wanaochungia katika hifadhi za taifa,misitu ya hifadhi ya jamii na mapori tengefu kuondoa mifugo yao kwani serikali haitamfumbia macho mfugaji yeyote au mkulima anayefanya shughuli za kibinadamu katika mazingira hayo.
Comments
Post a Comment