SIMBA SC YATAMBA KUENDELEZA REKODI YAO LEO



VINARA wa Ligi Kuu Tanzania bara, Simba wanatarajiwa kuendeleza rekodi yao ya kufanya vizuri bila kupoteza katika mchezo dhidi ya Mbao FC utakaochezwa leo kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.

Simba inajivunia kwa kila kitu. Inaongoza kileleni kwa pointi 23 katika michezo tisa iliyocheza kati ya hiyo imeshinda saba, imepata sare mbili, ikiwa na jumla ya mabao ya kufunga 17 na kuruhusu kufungwa matatu pekee.

Timu hiyo inajivunia mchezaji wake Shizza Kichuya akiongoza katika safu ya ushambuliaji kwa kufunga mabao saba peke yake hadi sasa, huku wengine katika timu nyingine wakifunga kuanzia manne. Hiyo ni kabla ya matokeo ya jana.

Iwapo itaendeleza ushindi itajiwekea rekodi ya kucheza michezo 10 bila kupoteza. Lakini pia, macho yataendelea kuwatazama washambuliaji wake wenye uchu wa kufunga wakati wote ambao ni Kichuya, Ibrahim Ajib na Laudit Mavugo.

Kocha Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja alisema kuwa ikiwa kikosi chake kitaendeleza umoja ilionao sasa, basi njia itakuwa nyeupe ya kushinda kila mchezo.
“Kila mchezo ni muhimu kwetu. Inahitajika umoja uwanjani na kujituma ili kupata matokeo,” alisema.

Inacheza na Mbao FC ambao bado wageni wa ligi lakini wamekuwa wakijitahidi kufanya vizuri katika matokeo yao yaliyopita.

Mbao sio timu ya kuibeza, ikiwa ugenini iliifunga Ruvu Shooting mabao 4-1 kwenye uwanja wa Mlandizi, Pwani, ikailazimisha Mtibwa Sugar sare ya bao 1-1 Manungu, hivi karibuni.

Timu hiyo imecheza michezo 10, imeshinda mitatu, imepata sare tatu na kupoteza minne na kufikisha pointi 12 ikishika nafasi ya nane.

Comments

Popular posts from this blog

AZAM FC,SIMBA SC ZAFANYA KUFURU USAJILI DIRISHA DOGO