AZAM FC,SIMBA SC ZAFANYA KUFURU USAJILI DIRISHA DOGO
WAKATI dirisha dogo la usajili wa Ligi Kuu Bara likifungwa saa sita usiku kuamkia leo, Simba na Azam FC zimeonekana kuwa na ‘vurugu’ nyingi katika kusajili wachezaji wa kimataifa na kitaifa katika kufanya marekebisho ya vikosi vyao tofauti na wapinzani wao kwenye ligi.
Mbali na timu hizo, Mbeya City imeonekana kujipanga pia kwa kusajili wachezaji wengi wa kimataifa kulinganisha na misimu iliyopita tangu imeanza kushiriki Ligi Kuu.
Kwa upande wa mabingwa watetezi, Yanga, mpaka jana jioni walifanya usajili wa wachezaji wawili pekee Justine Zulu wa Zambia na Emmanuel Martin kutoka Zanzibar na kuachana na Mbuyu Twite.
Hata hivyo, idadi ya wachezaji iliowasajili inaweza kuongeza ama kubaki hiyo hiyo kwani mpaka jana jioni taarifa zilidai kulikuwa na kikao kizito kuhusu usajili. Mzunguko wa pili wa ligi hiyo unatarajiwa kuanza kesho na macho ya wengi yanatamani kuona namna ambavyo usajili wa timu hizo utakavyoleta matunda, kila mmoja akionesha wazi kuwa anarudi kushindana na sio kusindikiza.
Simba imemsajili kiungo wa Ghana, James Kotei, kipa Daniel Agyei kutoka Medeama ya Ghana, Juma Luizio aliyekuwa Zesco United na Pastory Athanas kutoka Stand United huku ikipandisha wachezaji wawili kutoka kwenye timu yake ya vijana nahodha Moses Kitundu na beki Vincent Costa.
Taarifa ya Simba kwa vyombo vya habari jana ilisema katika kuimarisha kikosi chake timu hiyo imewatoa kwa mkopo Awadh Juma na Malika Ndeule waliokwenda Mwadui ya Shinyanga, Emmanuel Semwanza aliyekwenda kwa mkopo Ma- jimaji huku ikimrudisha Ame Ally ‘Zungu’ kwenye klabu yake ya Azam.
Zungu ametolewa tena kwa mkopo Kagera Sugar. Aidha Simba imeachana na kipa wake M-Ivory Coast, Vincent Angban na kiungo kutoka Congo DR, Mussa Ndusha. Kwa upande wa Azam, FC imesajili wachezaji Joseph Mahundi kutoka Mbeya City, Yahaya Mohamed, Samweli Afful, Daniel Agyei, Yakubu Mohammed (Ghana), Abdul Mohamed, Stephan Mpondo wa Cameroon.
Imeachana na Jean Mugiraneza ambaye anadaiwa kupata timu Vietnam. Pia, mapema iliwaacha Paschal Wawa, Michael Bolou na Thomas Renaldo wa Ivory Coast. Huenda kuna wazawa wengine watajulikana kuanzia leo. Miongoni mwa wachezaji wengine waliowahi kutajwa kuwa watapelekwa timu nyingine kwa mkopo ni Malimi Busungu na Antony Mateo.
Bado klabu hiyo imekuwa ikifanya mambo yake kwa usiri mkubwa pengine leo wataweka wazi. Aidha, Mbeya City pia imefanya kufuru kwa kuwasajili washambuliaji Mrisho Ngassa na wageni watatu ambao ni Tsipa Leonard kutoka Caps United ya Zimbabwe, Waganda Tito Okello, Hood Mayanja pamoja na beki William Otong ambao waliichezea African Lyon mzunguko wa kwanza wa ligi.
Kwa upande wa Mwadui imesajili wachezaji watano ambao ni Awadh Juma na Malika Ndeule (kwa mkopo Simba), Razack Khalfan (aliyekuwa kwa mkopo Singida United), Abdallah Seif (Azam) na Meshack Abel (African Lyon).
Nayo JKT Ruvu imefanya usajili wa wachezaji sita Edward Songo kutoka JKT Mlale, Edward Charles kutoka Geita Gold, huku wakimrejesha mshambuliaji Husein Bunu, Ally Bilal, Benjamin Magulu na Renatus Ambrose.
Comments
Post a Comment